Kwanini Marekani imebadili msimamo kuhusu mataifa yanayoongozwa kijeshi Afrika Magharibi?

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
- Author, Paul Melly
- Nafasi, Mchambuzi Afrika
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Marekani inaonekana kubadili msimamo wa sera zake kuhusu mataifa matatu ya Afrika Magharibi yanayokabiliana na wanamgambo wenye itikadi kali za kidini na ambayo serikali zao za kijeshi zimekatiza ushirikiano wa ulinzi na nUfaransa na badala yake kugeukia Urusi.
Wizara ya mambo ya nje ilitangaza kuwa Nick Checker, mkuu wa Ofisi yake ya Masuala ya Afrika, atazuru mji mkuu wa Mali Bamako ili kuwasilisha "heshima ya Marekani kwa mamlaka ya Mali" na kutayarisha "njia mpya" katika mahusiano, na kuweka kando "makosa ya sera zilizopita".
Marekani pia inatarajia kushirikiana na washirika wa Mali, nchi jirani za Burkina Faso na Niger, "katika usalama wa pamoja na maslahi ya kiuchumi".
Haipo katika ajenda ni wasiwasi wa muda mrefu wa Marekani kwa demokrasia na haki za binadamu. Utawala wa Biden ulikuwa umesitisha ushirikiano wa kijeshi baada ya mapinduzi kuwaondoa marais waliochaguliwa wa nchi zote tatu kati ya 2020 na 2023, huku Mohamed Bazoum wa Niger akiwa bado amefungwa katika makazi yake mwenyewe.
Kauli hiyo ya Marekani inaweka wazi mabadiliko makubwa ya sera ambayo yalizidi kudhihirika katika kipindi cha miezi 12 tangu Donald Trump arejee Ikulu ya Marekani.
Mabadiliko yalianza kwa kufungwa kwa USAID - shirika muhimu la kutoa msaada wa maendeleo katika kanda hiyo - siku chache baada ya rais kuapishwa kwa muhula mpya.
Hii ilifuatiwa na ishara za mara kwa mara za kuzingatia usalama na madini, huku maendeleo na utawala ukiwekwa kando.
Tangazo la ziara ya Checker linakwenda mbali zaidi katika kutangaza waziwazi heshima ya uhuru wa Mali. Ujumbe huo utasikika mjini Bamako na miji mikuu ya washirika, ambako viongozi wa kijeshi wamejenga mvuto wao kwa kugonga kaulimbiu za Waafrika na kukataa mamlaka ya zamani ya kikoloni Ufaransa.
Kiongozi wa kijeshi wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traoré, anajinadi kama mpinga "ubeberu" na "ukoloni mamboleo". Kupitia utangazaji mkubwa wa mitandao ya kijamii, amepata uungwaji mkono mkubwa kwa msimamo huu na umaarufu wa kibinafsi miongoni mwa vijana kote barani na kwingineko.
Utawala wa Trump umeweka wazi kwamba haujali na tawala zisizofuata mfumo wa kikatiba wa kuchagua serikali ya kiraia.
Massad Boulos, mshauri mkuu wa Afrika katika idara ya serikali na mhirika wa karibu wa Trump, mwaka jana aliliambia gazeti la Ufaransa Le Monde: "Demokrasia inathaminiwa kila mara, lakini sera yetu si kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine. Watu wako huru kuchagua mfumo wowote unaowafaa."
Mtazamo huu unaashiria mabadiliko makubwa.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wakati wa enzi ya Biden Jenerali Michael Langley, mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Marekani la Afrika (Africom) kutoka 2022 hadi 2025, alisisitiza umuhimu wa utawala bora na masuala ya mazingira, kama hatua muhimu kuelekea kupata msaada wa kijeshi.
Hata hivyo mwaka jana, baada ya Trump kurejea katika kiti cha urais, alisema kuwa kuunga mkono vita dhidi ya ugaidi sasa ndio jambo kuu.
Na hilo linaonekana kuwa jambo la kipaumbele katika Afrika Magharibi, ujumbe uliosisitizwa tena na Rudolph Attalah, afisa mkuu wa kukabiliana na ugaidi, alipotembelea Bamako mwaka jana.
Baadaye mwezi uliopita naibu mkuu wa Africom, Jenerali John Brennan, alithibitisha kwamba Marekani inaendelea kuunga mkono kikamilifu nchi hizo tatu zinazotawaliwa kijeshi katika mapambano yao dhidi ya makundi ya kijihadi, na hasa Islamic State.
Lengo la mabadiliko ya mtazamo wa Trumplinaonekana kuwa kubwa sana.
Marekani, kama Ulaya, ina wasiwasi mkubwa kuhusu tishio la usalama la muda mrefu linaloletwa na makundi ya kijihadi yanayohudumu katika eneo lote la Sahel - eneo lenye ukame kusini mwa Jangwa la Sahara. Kulingana na wachambuzi, eneo hilo sasa linachangia nusu ya vifo vyote vya ugaidi duniani.
Ingawa karibu majeruhi wote ni wa ndani, kuna wasiwasi nchini Marekani kwamba kushindwa kwa serikali kudhibiti sehemu kubwa ya nchi kunaweza kutoa mwanya wa kuibuka kwa maeneo salama kwa makundi ya kijihadi kujiendeleza zaidi na na kutanua wigo wao.
Wanadiplomasia na wachambuzi sasa wanaelezea eneo hilo kama "kitovu cha ugaidi wa kimataifa", ambacho kinaweza kutoa tishio la muda mrefu la kimataifa.
Katika "eneo la mpakani", ambapo Mali, Burkina na Niger hukutana, mrengo wa kundi la Afrika Magharibi la Dola ya Kiislamu (Jimbo la Kiislamu katika Jangwa la Sahara, ISGS) linafanya kazi sana.
Kundi hilo jipya wiki iliyopita lilifanywa shambulio dhidi ya uwanja wa ndege wa Niamey, mji mkuu wa Niger.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Shughuli za makundi ya kijihadi pia ni tishio kwa usafirishaji nje wa madini ya thamani yatishio kwa Sahel kuuza nje madini ya thamani au muhimu kimkakati: eneo hilo ni mzalishaji mkuu wa dhahabu na Mali pia inazalisha lithiamu - kiungo muhimu katika betri zinazoweza kuchajiwa tena na pia kutumika katika baadhi ya dawa - wakati Niger ina akiba kubwa ya urani.
Serikali ya kijeshi ya Niger imechukua udhibiti wa mgodi mkuu wa uranium nchini humo kutoka kwa mhudumu wa muda mrefu wa Ufaransa, Orano, na sasa inapanga Urusi kama mshirika wake mpya katika sekta hiyo.
Utawala wa Trump pia unaonekana kuwa na wasiwasi wa kutoiacha Urusi kuchukua nafasi ya mshirika pekee wa ulinzi wa nje wa nchi hizo tatu.
Tofauti na jumuiya ya kanda ya Afrika Magharibi Ecowas, Ufaransa, EU na utawala wa Biden, Ikulu ya White House ya leo haizingatii uwepo wa jeshi la Urusi kama tishio kwa utulivu wa kikanda au haki za binadamu. Urusi imetuma takriban wakandarasi 1,000 wa usalama nchini Mali, wakiwa na vikosi vidogo vya mamluki au wanajeshi wa kawaida nchini Burkina Faso na Niger.
Kumekuwa na madai mengi ya unyanyasaji uliofanywa na Warusi, haswa nchini Mali.
Attalah alipozuru Bamako, aliashiria kwamba Washington ilikuwa haitilii maanani ushiriki wa kijeshi wa Moscow Afrika Magharibi.
Inaonekana kwamba Washington haitaki tena kuacha uwanja ushawishi wa Urusi pekee na sasa inataka kusawazisha hilo na ushirikiano wake wa usalama.
Bado, hii itakuwa kwa masharti ambayo hayatavuruga msingi wa kisiasa wa Trump, ambaye ameahidi mara kwa mara kukomesha ushiriki wa Amerika katika "vita vya milele" nje ya nchi. Hii haihusu wanajeshi walio chini - pengine kwa timu za mafunzo za mara kwa mara.
Brennan wa Africom anasema Marekani inazipa Mali, Burkina na Niger msaada wa kijasusi na vidokezo kuhusu uwezekano wa usambazaji wa silaha.
Lakini Washington haina mpango wa kupeleka tena vikosivyake au kufungua tena kituo kikubwa cha ndege zisizo na rubani ilichojenga Agadez, Niger, ambapo ilikuwa na takriban wanajeshi 800. Wanajeshi hao waliwafukuza baada ya serikali ya Biden kushinikiza kurejeshwa kwa mfumo wa kidemokrasia.
Kufuatia wimbi la mapinduzi, Ecowas ilijaribu kuwashinikiza viongozi wa kijeshi kuweka wazi tarehe za chaguzi mpya.
Lakini Niger, Burkina na Mali zilijiondoa kwenye Jumuiya ya ECOWAS mwaka jana na kuunda Muungano wa Nchi za Sahel (AES).
Kwa sababu wao si wanachama tena, Ecowas haina jukumu la kushughulikia maadili yao ya utawala wa ndani.
Na hii imezikomboa nchi wanachama wake kadhaa zilizosalia kwao wenyewe kujaribu kujenga tena ushirikiano na nchi hizo tatu katika mapambano dhidi ya makundi ya kijihadi.
Hiki ni kipaumbele kikubwa kwa serikali katika kanda nzima, wakati ambapo wanamgambo wamekuwa wakipenya nje ya mipakani, kufanya mashambulizi au kujificha kaskazini mwa nchi kama vile Benin, Nigeria na Togo, Ghana na Ivory Coast.
Huku eneo hilo likikabiliwa na changamoto hii ya kutisha, ujasusi wa Marekani katika shabaha kuu, na pengine silaha za ziada pia, zinaweza kusaidia kupata ushindi wa haraka dhidi ya wanamgambo hao.
Lakini - kama vile mwongo mmoja wa Ufaransa wa kupeleka maelfu ya wanajeshi na nguvu za anga katika Sahel ilionyesha - njia za kijeshi za teknolojia ya hali ya juu pekee haziwezi kurejesha amani, isipokuwa matatizo magumu ya kijamii na kiuchumi katika eneo hili maskini sana la dunia pia yatashughulikiwa.















